MTOTO AFUNGIWA KWENYE BANDA LA MBUZI KWA MIAKA 10
Juni 21 ilikuwa ni siku ya kawaida kwa Mama Nancy mkazi wa Narok nchini Kenya, lakini ilifichua siri nzito ya mtoto aliyefichwa kwa miaka kumi katika banda la mbuzi.
Akiwa katika shughuli zake za nyumbani, mara akatokea mtoto mdogo wa jirani yake aitwaye Jane.
Binti huyo akaanza kucheza na wenzake kwa dakika kadhaa na mara akaacha michezo na kuanza kukimbia kuelekea nyumbani kwao.
Wenzake
wakamuuliza “mbona unakimbia wakati bado tunacheza”. Akajibu, “nakwenda
kwenye banda la mifugo kumpa chakula Ben. Muda umekimbia na hakuna mtu
nyumbani”.
Kwa
kauli hiyo, mwanamke huyo alitaka kujua iwapo Ben anaishi kwenye nyumba
ya jirani yake kwani ni miaka 10 imepita tangu amtie machoni.
“Ben
yupo na anaishi kwenye banda la mifugo. Huwa anahudumiwa na mama,
lakini kwa sasa mama hayupo na baba amekwenda kazini. Mimi nina jukumu
la kumpa chakula,” alijibu Jane.
Mama
huyo akapata shauku ya kumtembelea mtoto huyo kuona kinachoendelea kwa
jirani zake, Lo! anachokiona haamini macho yake; Mtoto Ben amefungwa kwa
kamba kwenye kigodoro chembamba akiwa hajiwezi kwa njaa.
Hivyo ndivyo alivyoibuliwa mtoto Ben baada ya kukaa katika banda la mbuzi kwa muda wa miaka 10 bila majirani kufahamu.
Ben,
ambaye kwa sasa ana miaka miaka 14 alizaliwa akiwa kiziwi, bubu na
ulemavu. Aibu ya kuzaa mtoto kama huyo ndiyo ilifanya wazazi wake
wamfungie kwenye zizi la wanyama kwa muda wa miaka 10 na wakihakikisha
hakuna jirani wala ndugu wa karibu anayefahamu juu ya tukio hilo.
Historia ya mtoto huyo
Kwa
mujibu wa baba mlezi Mr Jeremiah Mbusia, ambaye ni askari katika
Wizara ya Mali Asili, Narok Kenya, mtoto huyo siyo wake wa kuzaa bali
alifika katika nyumba hiyo miaka 12 iliyopita akiwa na mama yake wakati
huo mtoto huyo alikuwa na miaka minne.
Alilelewa
katika nyumba hiyo kwa miaka miwili na ndipo wazazi wake, yaani baba
yake wa kambo na mama yake mzazi wakaamua kumuweka katika kibanda kidogo
nje ya nyumba yao na hutumiwa kama zizi la mbuzi na kondoo.
Maisha ndani ya zizi
Akiwa kwenye zizi mtoto huyo aliwekewa godoro ukutani na mkono wake mmoja ulifungwa kwa kamba ukutani.
Ilikuwa
ni vigumu kuvumilia harufu kali kutoka katika zizi hilo kwani kulikuwa
na mchanganyiko wa kinyesi na mikojo ya binadamu na wanyama.
Wadogo
zake Ben walisema kuwa wazazi wao huwa wanamsafisha mtoto huyo wakati
wowote wanaotaka na kuwa anaweza kushinda na kinyesi au kulala nacho.
“Ni
mara chache kukuta akisafishwa mara mbili kwa siku. Kwa kawaida
husafishwa mara moja tu na wakati mwingine hasafishwi kabisa,” alisema
mtoto huyo.
Kwa nini ilikuwa rahisi kujulikana?
Ugunduzi
wa mtoto huyo ulitokana na ukweli kwamba mama yake aliamua kuondoka
nyumbani na kuacha familia nzima kutokana na ugomvi na mume wake.
Mama
huyo alikuwa akifanya siri ya kulinda mtoto huyo asijulikane hapo
nyumbani na alipoondoka watoto wenzake ndiyo walikuwa na jukumu la
kumlisha mwezao.
Kauli ya baba mlezi
Kwa kujibu wa baba wa kambo, mama wa mtoto huyo alikuwa hamtaki mwanaye kwani aliamini kwamba kuishi naye ni kuongeza mikosi.
Baada
ya kuishi pamoja walijikuta wakiwa wamezaa watoto watatu na mama huyo
aliona kuwa watoto hao ndio walikuwa muhimu katika maisha yake kuliko
Ben, ambaye alimzaa na mwanaume mwingine kabla ya kuolewa katika ndoa
rasmi.
“Mama
yake alikuwa hampendi na hata wazo la kumweka katika banda lilitoka
kwake. Aliamini kuwa kukaa naye ndani kama watoto wa kawaida ilikuwa ni
usumbufu na akitoa visingizio kwamba akikaa ndani anaweza kuvunja vitu
na kuwa anaweza kushika vitu vya hatari kama vile moto,” alijitetea baba
mlezi wa Ben.
“Tulikosana
na mama watoto kwa ugomvi wa kawaida tu katika familia, hiyo ilikuwa ni
miezi minne iliyopita, ajabu ni kwamba amenikimbia na kuniachia familia
akiwamo mtoto mlemavu.” “Nashindwa kumlea vizuri kwa kuwa natakiwa
kwenda katika mihangaiko yangu ndiyo maana wadogo zake walikuwa
wakimhudumia wakati sipo.”
Imefahamika
kuwa mwanamke huyo amekimbilia kwao eneo la Rimuru, Kenya ambapo ni kwa
wazazi wake na akiwaambia jamaa zake wa karibu kuwa hawezi kurudi
katika nyumba ya mume wake kwani hawapatani.
Kauli za majirani
Majirani
wanasema walikuwa wakifahamu kuwa nyumbani kwa jirani yao kuna mtoto
mwenye ulemavu wa akili lakini hawakumwona kwa muda mrefu.
“Tulikuwa
tukifahamu kwamba kuna mtoto mlemavu wa akili lakini katika kipindi cha
miaka 10 iliyopita hatukumwona. Tulidhani wamemhamishia sehemu
nyingine. Ilikuwani vigumu kusikia sauti kwa kuwa mtoto mwenyewe ni bubu
na kiziwi,” alisema jirani mmoja.
Kumuokoa Ben
Baada ya majirani kupata taarifa za kuwepo kwa mtoto huyo, walimuita mwandishi wa habari mmoja ili kushuhudia hali halisi.
Mwandishi
huyo alitoa taarifa polisi na pia kwa Mwenyekiti wa Baraza la Taifa la
watu wenye ulemavu Kenya, Dk David Ole Sankok na kwa pamoja walivamia
katika nyumba hiyo iliyopo Fanaka Estate, Narok na kumwokoa mtoto huyo
katika mateso.
Baada
ya kumtoa kwenye kibanda hicho waligundua kuwa hali ya mtoto huyo
haikuwa nzuri kwani alikuwa amepooza upande mmoja wa kushoto kutokana na
kulala kwa muda mrefu, viungo vyake vilikuwa vimejikunja kutokana na
kukosa lishe kwa siku nyingi na nywele zake zilibadilika rangi kutokana
na kutokaa kwenye mwanga wa jua kwa muda mrefu.
“Alikuwa
akitoa harufu kali, ilikuwa ni vigumu hata kumsogelea, lakini kwa kuwa
tulikuwa tumedhamiria kumwokoa ilibidi tufanye hivyo,” akasema Dk Ole
Sankok. “Tulimkuta katika mateso makubwa sana, eneo alilokuwa amelala
lilikuwa na kunguni, chawa na viroboto wengi,” anasema.
Anaongeza kuwa wadudu hao walipokuwa wakimsogelea kinywani alikuwa akiwatafuna na kuwameza kwani alikuwa na njaa muda wote.
“Nilipoona
hali hiyo nilijaribu kuondoa viroboto waliokuwa karibu na mdomo wake,
kwa kuwa alikuwa amewazoea sana na aliona ni kama kitoweo chake alitoa
sauti ya ukali kuashiria kwamba nisiwatoe, nilipojaribu kuwatoa kwa
nguvu alitaka kuniuma kwa meno,” alisema daktari huyo.
Wazazi
wa kijana huyo walikuwa hawaaniki godoro nje kwani hawakua na jingine
la kumtandikia pia walihofia majirani huenda wangehoji.
Huduma ya kwanza
Baada
ya kugunduliwa, Ben alipelekwa katika Hospitali ya Mji wa Narok kwa
ajili ya matibabu. Alipewa huduma za haraka ikiwa ni pamoja na huduma za
kurudisha afya mwilini kwa vyakula vya protini na vitamini.
Vilevile
alikuwa akianikwa juani mara kwa mara kwa lengo la kumrudishai
vitamini. Kwa kuwa mgongo wa mtoto huyo ulianza kutoa vidonda alipewa
matibabu ya vidonda.
“Mtoto
huyo alikuwa amepungua mwili kwa kiasi kikubwa ilikuwa unaweza kumbeba
kama mtoto mdogo. Hata rangi yake ya ngozi ilibadilika,” alisema Dk
Sankok, ambaye pia anaendesha kliniki binafsi katika mji wa Narok.
“Licha ya kuwa na umri wa miaka 14 alikuwa na kilo 15 pekee,” aliongeza.
Sankok
aliwahakikishia watu waliomzunguka mtoto huyo kwamba atamfikisha katika
kituo cha kulelea watoto wenye ulemavu wa akili na viungo na atampa
mazoezi ya kutosha kuhakikisha anarudi katika hali ya kawaida.
“Unajua
kuna wazazi ambao wana kawaida ya kuwaficha watoto wao kwa sababu wana
matatizo ya viungo ama ya akili. Hilo siyo jambo zuri hata kidogo,
watoto kama hao ni binadamu wa kawaida na wanatakiwa kulelewa kwa
misingi yote ya kibinadamu,” anasema.
Anasema
kama mzazi anaona hawezi kumhudumia mtoto kama huyo ni bora amfikishe
katika vituo vya kulea watu wa aina hiyo kuliko kumficha ndani na kumpa
mateso makubwa.
hadi wakenya..mamaaa
ReplyDelete